Mbunge wa kigoma mjini na kiongozi mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe na mke wake wamepata mtoto wa kike ambaye wamempa jina la Josina – Umm Kulthum.

Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa facebook amesimulia alichokutana nacho hospitalini saa chache kabla ya mke wake kujifungua, haya ni maneno yake.

Usiku wa kuamkia tarehe 26 Desemba 2016 mke wangu alipata uchungu wa uzazi. Nikampeleka hospitali moja hapa Masaki. Hakuweza kujifungua siku hiyo bali tulikaa hospitali mpaka tarehe 27 Desemba, saa moja dk 45 asubuhi alipojifungua mtoto wetu wa kike Josina- Umm Kulthum.

Masaa ya jioni tarehe 26/12/2016 nikiwa napiga soga na Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Msafiri Mtemelwa na shemeji yangu mmoja mbele ya hospitali, wakaja watu 3. Watu hao mmoja mwanaume na wengine wanawake walikuwa na mtoto mdogo.

Mwanaume huyu alikuwa amembeba mtoto akiwa na taharuki kubwa na mama mmoja mtu mzima na mwingine wa umri wa miaka 30 hivi walikuwa wakilia. Wakaingia hospitalini kwa kasi. Tukaambiana pale kuwa huyu binti atakuwa mahututi. Tukaendelea na soga.

Mara kina mama wale wakatoka, wanapiga mayowe “mtoto hana damu” na ilitakiwa damu ya haraka Group A+. Wenzangu hawakuwa group hilo au group linaloweza kupeana damu. Mimi sikuwa najua/kukumbuka Group langu.

Nikawaambia kina mama wale kuwa ngoja nijaribu kupima group langu na pia kuona kama damu yangu inaweza kuokoa maisha ya mtoto yule malaika za mungu. Nikaingia maabara nikapima. Baada ya dakika 10 Hivi nikaitwa kuambiwa damu yangu ni group sawa na mtoto yule na kwamba ni safi inafaa wanitoe muda ule ule ili kumuwahi mtoto. Nikatoa nusu lita muda ule ule.

Baadaye nikaenda kumjulia Hali mtoto yule, nikaambiwa anaitwa Rahma. Ana umri wa miaka 2 na miezi 3. Nikawatakia kheri wazazi wake ( kumbe yule mwanaume ndie baba wa mtoto na msichana mama yake. Yule bi mkubwa nadhani ni bibi ya Rahma, sina hakika).

Leo asubuhi baada ya mke wangu kujifungua, nikaenda kumwona Rahma wodini. Nimemkuta anaendelea vizuri, anakula na kuongea. Mola ampe umri mrefu zaidi yeye na wazazi wake. Amwondolee maradhi na akue katika maadili mema ya dini.

Namshukuru mola kuniweka mahala sahihi na wakati sahihi hivyo kuweza kufanya ibada hii ya kumsaidia binti Rahma. Lau kama sikuwa nimechagua jina la binti yangu mapema, ningemwita Rahma. Hata hivyo inshallah Rahma atakuwa dada yake Umm Kulthum-Josina.

Naishauri Serikali itengeneze kanuni za kuhakikisha kila hospitali inakuwa na akiba ya damu ya kutosha na mgonjwa mwenye kuhitaji apewe kwanza damu kabla ya kutafuta watu wa kuchangia kiwango husika.

Juhudi za kuchangia damu kwa hiari ziongezeke kama tufanyavyo wanachama wa ACT Wazalendo ambao kila mwaka Wiki ya kwanza ya Mwezi Mei hujitolea damu kwa hiari kwenye hospitali za umma nchini kote.

Aidha nimepata somo kubwa kwamba ni muhimu Sana kujua Group lako la damu na kuwa na kumbukumbu nalo kwani inaokoa muda pindi damu ikitakiwa kwa haraka. Sasa najua Group langu, ilikuwa ni makosa makubwa na uzembe wa hali ya juu kwangu kutojua ‘ blood group ‘ yangu. Nawasihi Watanzania wenzangu na mie msiojua blood group, mjue sasa kwani hatujui Siku wala Saa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *