Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto ameitaka serikali iboreshe sekta ya madini ili kuisaidia nchi kunufaika na madini yaliyopo nchini.

Zitto ambaye ni kiongozi wa ACT – Wazalendo ametoa kauli hiyo wakati akimnadi mgombea wa ACT-Wazalendo, Ibrahim Masele katika kampeni za uchaguzi mdogo katika kata ya Isagehe, Kahama Mjini.

Amesema, tangu Tanzania imeanza kuchimba dhahabu kwa kutumia kampuni kubwa ( uchimbaji mkubwa ) imeshauza nje dhahabu ya thamani zaidi ya sh trilioni 45 huku bajeti ya Tanzania ya mwaka huu 2016/17 ni sh 29 trilioni.

Hivyo alisema tangu mwaka 1997 uchimbaji mkubwa wa madini ulipoanza nchi imeuza madini nje lakini mauzo hayo ya nje hayafaidishi nchi.

Kutokana na mazingira hayo aliwataka wananchi wa Isagehe kumchagua diwani wa ACT ili kuendeleza mapambano yatakayosaidia wananchi .

Alisema mwaka 2007, waliibua hoja ya ufisadi wa Mgodi wa Buzwagi, wakati huo ilikuwa kila mgodi kwenye mkataba unatoa dola 200,000 kwa mwaka kwenye halmashauri yenye mgodi kama mapato ya ndani.

Zitto alisema baada ya mapambano kuhusu Buzwagi iliundwa Kamati ya Bomani na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne Dk Jakaya Kikwete na ilizalisha Sera mpya ya Madini ya mwaka 2009 na Sheria mpya ya Madini ya mwaka 2010 lakini licha ya kazi kubwa walioifanya wakati ule ya kuleta sera na sheria mpya ya madini lakini nchi bado hainufaiki na rasilimali hiyo.

Baada ya kufanya mabadiliko makubwa ya sheria ya madini, Aprili 2010 ikaonekana kampuni zote zitalipa ushuru wa huduma asilimia 0.3, ya mapato ambayo kampuni inapata badala ya kulipa dola 200,000.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *