Yanga leo imetoa kichapo cha kufa mtu baada ya kuikandamiza Kagera Sugar 6-2 kwenye mechi ya ligi kuu Tanzania Bara iliyofanyika katika uwanja wa Kaitaba mjini Bokoba mkoani Kagera.

Ushindi huo wa Yanga unaifanya timu hiyo ifikishe pointi 21 baada ya kucheza mechi 10, ingawa inaendelea kukaa nafasi ya tatu nyuma ya Stand United yenye pointi 23 na Simba SC 26.

Hadi mapumziko Yanga walikuwa wanaongoza 3-1kabla ya mvua ya magoli kuibuka kipindi cha pili.

Yanga walilazimika kutoka nyuma baada ya Mbaraka Yussuf kutangulia kuifungia Kagera Sugar dakika ya tatu.

Donald Ngoma akaisawazishia Yanga baada ya shambulizi la haraka akimalizia kwa kichwa krosi ya Simon Msuva dakika ya nne mbele.

Msuva akafunga mwenyewe dakika ya 21 kuipatia Yanga bao la pili baada ya kumalizia mpira uliotemwa na kipa Hussein Sharrif ‘Cassilas’ kufuatia shuti la kiungo Haruna Niyonzima.

Obrey Chirwa akaifungia Yanga bao la tatu dakika ya 26 akimalizia mpira uliotemwa na Casillas tena baada ya shuti la Ngoma.

Kipindi cha pili, Kagera wakaanza vizuri na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 49, mfungaji yule yule Mbaraka Yussuf aliyetumia makosa ya mabeki wa Yanga.

Yanga wakafanikiwa kupata bao la nne lililofungwa na Deus Kaseke dakika ya 58 kwa shuti akimalizia krosi ya Msuva.

Chirwa akaifungia Yanga bao la tano akimalizia mpira uliotemwa na kipa Burhan baada ya shuti la Ngoma.

Donald Ngoma akakamilisha ushindi mnono wa Yanga leo kwa kufunga bao la sita dakika ya 64 baada ya kuambaa na mpira na kumchambua Burhan kufuatia pasi ya Haruna Niyonzima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *