Yanga na Azam leo zitakutana kwenye mchezo wa tatu wa Kundi A kwenye michuano ya Mapinduzi katika Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.

Timu hizo leo zinakutana mara 27 kwenye mashindano yote, ambapo kwenye Ligi Kuu wamecheza mechi 17 Yanga wameshinda mara tano, Azam nao wameshinda mara tano, wametoka sare mara saba, timu hizo zimefungana kwa idadi ya mabao 25.

Kwa upande wa Kombe la Mapinduzi, timu hizo zimekutana mara mbili, awali zilikutana mwaka 2012, ambapo Azam FC inaonekana kuwa na rekodi nzuri pale ilipoifunga Yanga kwa mabao 3-0 Azam kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 mwaka 2016 katika michuano hiyo.

Hivyo, pamoja na Yanga kuwa na tiketi yake mkononi ya kucheza nusu fainali, mchezo huo kwao utakuwa wa kulinda heshima na kutaka kulipa kisasi cha kufungwa na Azam FC mwaka 2012, hivyo Wana lambalamba hao wasitarajie mteremko kutroka kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Yanga ndio inaongoza kundi lao wakiwa na pointi sita mbele ya Azam wenye pointi nne, huku Jamhuri ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi yake moja wakati Zimamoto haijambulia pointi baada ya kila timu kucheza mechi mbili.

Azam FC inahitaji sare tu ili iweze kufikisha pointi tano, ambazo hazitaweza kufikiwa na timu nyingine yoyote ukiondoa Yanga, ambao tayari imeshasonga mbele. Kikosi cha Azam kinatarajiwa kusheheni wachezaji wa kimataifa kama Yahaya Mohamed, Enock Agyei, Yakubu, na wengine, huku Yanga ikiwatumia zaidi Thaban Kamusoko, Donald Ngoma, Tambwe na Msuva katika kupata mabao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *