Mabingwa wa soka nchini, Yanga imeshindwa kulipiza kisasi dhidi ya TP Mazembe baada ya kukubali kichapo cha  3-1 kwenye mechi ya kombe la Shirikisho Afrika kundi A iliyofanyika katika uwanja wa Stade de TP mjini Lubumbashi.

Magoli ya TP Mazembe yamefungwa na Bolingi katika dakika ya 28 huku magoli mengine yakifungwa na Kalaba mnamo dakika ya 55 na 63 huku goli la Yanga likifungwa na mshambuliaji Amissi Tambwe dakika ya 74.

TP Mazembe inaongoza kundi hilo huku tayari ikiwa imeshajihakikishia nafasi ya kucheza nusu fainali ya michuano hiyo.

Yanga inatarajiwa kurudi nchini kesho kwa ajili ya kujiandaa na mechi za ligi kuu Tanzania Bara msimu mpya ulionza wiki iliyopita.

TP Mazembe iliyomaliza ikiwa kileleni mwa kundi A imeambatana na timu ya Mo Bejaia ya Algeria kwenye nusu fainali za kombe hilo baada ya timu hiyo ya Algeria kuifunga Medeama ya Ghana kwa bao 1-0 kwenye mchezo mwingine wa kundi hilo.

Mo Bejaia imefanikiwa kutinga nusu fainali kwa sheria ya ‘matokeo baina yenu’ a.k.a head-to-head rule baada ya kufungana kwa pointi ni Medeama.

Mo Bejaia itakutana na FUS Rabat baada ya timu hiyo kutoka suluhu ya 0-0 na bingwa mtetezi Etoile du Sahel ya Tunisia kwenye pambano la kundi B.

Etoile du Sahel ambayo pia imefanikiwa kutinga nusu fainali itakutana na TP Mazembe baada ya Etoile kuambulia nafasi ya pili kwenye kundi B.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *