Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imezindua mchakato wa kujenga mfumo unganishi wa taarifa za ardhi kwa njia ya mtandao wa internet (ILMIS) ambao unatarajiwa kuwa msaada mkubwa katika kutatua migogoro ya ardhi hapa nchini.

Mfumo huo ambao pia utahusisha upigaji picha wa jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kuandaa ramani ya jiji unatarajia kuanza kufanya kazi wilaya ya Kinondoni  kisha wilaya zote za mkoa wa Dar na baadaye katika kanda zingine.

Waziri wa wizara hiyo Mhe.Wiliam Lukuvu amesema mfumo huu utawezesha kuwa na uhakika wa kupata kwa haraka taarifa za wamiliki halali wa viwanja na kupunguza au kumaliza migogoro inayohusu viwanja kutolewa mara mbili.

Pia Waziri Lukuvi amefafanua kuwa chini ya mfumo huo haitakuwa rahisi kwa mtu kughushi nyaraka za umiliki wa viwanja ambavyo nyaraka zake zimepotea na kutambua maeneo yaliyopagwa kwa shughuli maalum ili kudhibiti udanganyifu katika sekta ya ardhi.

Kwa upande wake katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk. Yamungu Kayandabila amesema kwamba serikali imeamua kujenga mfumo huo ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya taarifa za sekta ya ardhi ambalo limesababisha uwepo wa hitaji la mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu za ardhi na mfumo wa kufuatilia pango la kodi ya ardhi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *