Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema wizara yake inafanya utafiti ambao utawezesha kujengwa kwa nyumba zenye gharama nafuu kwa ajili ya wananchi wa kawaida.

Lukuvi amesema wanafanya tafiti mbili za ujenzi wa dari la gharama nafuu katika nyumba za ghorofa na tafiti ya matumizi ya nishati katika uzalishaji wa vifaa na ujenzi wa nyumba zimekamilika.

Alikuwa akizungumza kwenye warsha kuhusu jukumu la vyombo vya habari katika kutoa elimu juu ya sheria, kanuni na taratibu katika utawala wa ardhi ili kusaidia kutatua migogoro ya ardhi iliyoandaliwa na Mpango wa Urasimishaji Ardhi (LTSP) unaotekelezwana wizara yake.

Amesema kwa sasa nyumba zinazojengwa na Shirika la Nyumba pamoja na kampuni ya Watumishi sio nyumba zenye gharama nafuu; na wananchi wenye kipato cha kawaida hawawezi kuzimudu.

Amesema wanasaka teknolojia hiyo ili nyumba hizo ziwe nafuu kwa teknolojia, gharama lakini zenye ubora unaokidhi. Akielezea mafaniko mengine ya wizara hiyo, alisema katika uzalishaji wa vifaa Wakala (NHBRA) umetengeneza mashine 41 za matofali ya kufungamana na umezalisha vigae 10,800 na kofia 240.

Pia amesema katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuwezesha mitaji na mikopo ya nyumba, mikopo ya nyumba yenye thamani ya Sh bilioni 374. 5 imetolewa kwa wananchi 4,065.

Vile vile ameongeza kwa kusema kuwa jumla ya benki 27 kati ya benki 54 zilizopo nchini zimetoa mikopo kwa wananchi na kati ya benki 14 zenye hisa TMRC ni Benki Nane zilitoa mikopo ya nyumba yenye thamani ya Sh bilioni 45.9 kwa wananchi 579.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *