Wenyeviti 50 wa Serikali za Mitaa wa Chama cha Wananchi, CUF Mkoa wa Dar es Salaam wametangaza kuunga mkono uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF la upande wa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.

Wenyeviti hao wamesema wanaunga mkono maamuzi ya kuwavua uanachama Wabunge wanne wa viti maalumu na madiwani wawili wa CUF kutokana na ukweli kwamba viongozi hao wamekisaliti chama.

Wakiwakilisha wenzao 36 wenyeviti 14 kutoka mitaa mbalimbali ya halmashauri za manispaa tano za jiji la Dar es Salaam wamesema wamefikia hatua hiyo baada ya kuridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Profesa Lipumba.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake 14 Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Keko Mwanga B, Shilingi Shilingi amesema wanaunga mkono uamuzi wote wa Baraza Kuu la Uongozi kwa kuwa Wabunge hao wamebainika kukihujumu chama hicho.

Shilingi ameongeza kuwa, wanamtambua Maalim Seif Sharif Hamad kama Katibu Mkuu lakini kwa sasa nafasi yake inakaimiwa na Magdalena Sakaya kutokana Maalim Seif kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya CUF.

Mbali na hilo Shilingi amewataka watu wanaoingilia mgogoro wa chama hicho kuacha mara moja na kwamba mgogoro ni wa Kikatiba na suala hilo lipo Mahakamani na kwamba, muda si mrefu uamuzi utatolewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *