Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), katika utafiti wao, wamebaini ugonjwa uliobuka katika mikoa ya Dodoma na Manyara hivi karibuni na kuua watu, unasababishwa na sumu ya kuvu inayoshambulia ini.

Jumla ya wagonjwa 54 walisharipotiwa kuathiriwa na ugonjwa huo katika mikoa hiyo na kati yao 14 wameshapoteza maisha sawa na asilimia 20, hali ambayo Serikali imebainisha kuwa ni changamoto kubwa katika afya.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kuhusu mwenendo wa hali ya ugonjwa huo katika maeneo yaliyoathirika.

Waziri huyo amesema tangu kuibuka kwa ugonjwa huo Serikali ilishirikiana na taasisi zake ikiwemo TFDA, Ofisi ya Mkemia Mkuu pamoja na wadau wa sekta ya kilimo na mifugo, mashirika ya kimataifa ikiwemo WHO na kuuchunguza kwa undani ugonjwa huo.

Waziri amesema Katika uchunguzi huo waliangalia nafaka hasa mahindi yaliyokuwa yanatumiwa na jamii iliyoathirika na kubaini kuwa nafaka hizo zilikuwa zimeharibika kwa kubadilika rangi na kuoza, pia wamegundua jamii hizo, zimekuwa zikihifadhi vyakula kwa mtindo usioridhisha.

Kati ya sampuli 115,52 sawa na asilimia 45 zilionesha kuwa na uchafu wa sumu ya kuvu kwa kiasi kisichokubalika kwa mujibu wa viwango vya kimataifa ambacho ni microgram isiyozidi tano kwa kilo moja ya nafaka.

Pia waziri Ummy Mwalimu ameeleza kuwa asilimia kubwa ya sampuli hizo zilipopimwa, zilionekana kuwa na uchafu wa sumu ya kuvu kwa kiwango cha microgram 5.7 hadi 204.5 kwa kilo moja ya nafaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *