Waziri  wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amemjia juu Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema kwa kauli yake kwamba wabunge wanaogopa kujadili mauaji yanayoendelea Kibiti wakihofia yatahamia kwao.

Mwigulu alichukizwa na kauli hiyo jana bungeni wakati wa mjadala kuhusu kuridhia   itifaki ya udhibiti wa mazingira ya bahari na ukanda wa Pwani ya Magharibi ya Bahari ya Hindi kutokana na vyanzo na shughuli zinazofanyika nchi kavu.

Nyingine ni    itifaki ya Kusimamia Upatikanaji na Mgawanyo sahihi wa faida zinazotokana na matumizi ya rasimali za  jenetiki.

Wakati akichangia, Lema alisema   wabunge wasishangae mauaji yanayotokea Kibiti yakisambaa nchi nzima.

Akijibu, Waziri Mwigulu pamoja na mambo mengine, alisema Serikali haitaacha eneo hata moja la nchi likatawaliwe na wahalifu.

Wilaya za Mkoa wa Pwani za Rufiji, Kibiti na Mkuranga zimekumbwa na mauaji  ya viongozi wa vijiji na vitongoji tangu Mei  mwaka jana na hadi sasa  zaidi ya watu 30 wameuawa.

Mauaji mengi yamekuwa yakifanyika usiku kwenye nyumba za viongozi na watu wengine ambao wamewahi kushika uongozi, idara ya maliasili na polisi.

Bunge jana liliridhia itifaki ya udhibiti wa mazingira ya Bahari na Ukanda wa Pwani ya Magharibi ya Bahari ya Hindi kutokana na vyanzo na shughuli zinazofanyika nchi kavu na ile ya itifaki ya Kusimamia Upatikanaji na Mgawanyo sahihi wa faida zinazotokana na matumizi ya rasimali za  jenetiki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *