Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ameipongeza kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Arusha chini ya mwenyekiti Mrisho Gambo ambaye ni mkuu wa mkoa kwa kuendelea kufanikisha ujenzi wa nyumba za Askari.
Waziri Mwigulu ametoa pongezi hizo baada ya kutembelea na kujionea ujenzi wa nyumba za askari ambazo ziliungua kwa moto mwezi Septemba na kuacha familia za askari zaidi ya 13 zikiwa bila makazi pamoja na vitu vya ndani.
Pamoja na shukrani hizo lakini Mwigulu amesema kuwa suala la makazi bora kwa askari ni kipaumbelele cha serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli hivyo wataendelea kuboresha makazi yao kadri inavyowezekana.
Ujenzi wa nyumba hizo ulianza Oktoba 2 mwaka huu ambapo jumla ya nyumba 29 za askari katika kambi iliyoathirika na moto zinajengwa. Wakati huo nyumba Saba zinajengwa kwenye kituo kidogo cha Polisi Morombo kata ya Murieti na zipo katika hatua ya msingi.
Rais Magufuli aliguswa na tukio hilo na kutoa pole pamoja na mchango wake kama serikali ili kuwezesha ujenzi wa nyumba mpya. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha RPC Charles Mkumbo ameendelea kuwashukuru wadau kwa kujitolea na kuwaomba kuendelea kushirikiana na jeshi la Polisi kuboresha makazi ya Askari hali ambayo itaongeza morali ya kazi.