Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango leo anatarajiwa kuwasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Serikali ya takribani Sh trilioni 31.6 kwa mwaka ujao wa fedha – 2017/18.

Baada ya kusomwa kwa bajeti hiyo, baadhi ya mambo yanayotarajiwa kuibuliwa wakati wa mjadala, ni pamoja na deni la taifa ambalo limeongezeka kwa kasi siku za usoni, misamaha ya kodi hasa kwenye sekta ya madini, upanuzi wa vyanzo vya kodi na hazina kutotoa fedha zinazotengwa kwa wizara mbalimbali.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2015/16 hadi Juni 2016, deni la taifa lilifikia Sh trilioni 41 ikilinganishwa na Sh trilioni 33 za deni hilo Juni 2015.

Ripoti hiyo inasema kiasi cha deni hilo la Juni 2016, hakijajumuisha Sh trilioni nane ambalo ni deni katika hifadhi za jamii.

Kwa mwaka ujao wa fedha, Serikali inatarajia kutumia Sh trilioni tisa kulipa deni la taifa lililoiva.

Kwa upande wa misamaha ya kodi ambayo pia inatarajiwa kutawala mjadala huo, ripoti ya CAG inaonyesha hadi Mei 2016 ilibaini kuwapo kwa matumizi mabaya ya msamaha wa kodi wa Sh bilioni 3.46 ambao ulitolewa kwa walengwa wawili walioagiza magari 238.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *