Waziri Mkuu wa Uhispania, Mariano Rajoy amemtaka Kiongozi wa Catalonia Carles Puigdemont kuachana na mpango wa kujitenga kama sharti la kuanzisha mazungumzo.
Jana Uhispania ilikataa wito wa kiongozi huyo wa kufanyika mazungumzo ili kutafuta njia ya kumaliza mzozo wa kisiasa uliochochewa na kura ya maoni kuhusu uhuru wa jimbo la Catalonia iliyofanyika Jumapili iliyopita.
Rajoy amesema kama kiongozi huyo wa Catalonia anataka mazungumzo au anataka kutuma wapatanishi, inampasa kwanza afuate sheria.
Kiongozi wa Catalonia amemshutumu Mfalme Felipe wa Sita wa Uhispania kwa kuwapuuza watu wa Catalonia baada ya kuwatolea wito wa kuachana na juhudi zao za kujipatia uhuru wa jimbo hilo.
Hata hivyo hotuba ya Mfalme Felipe, haikutaja chochote kuhusu watu waliojeruhiwa katika ghasia zilizozuka wakati wa kura hiyo ya maoni.