Waziri mkuu wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amezitaka taasisi za serikali kuanza mikakati madhubuti ya kubadili mfumo wa kupikia na kuweka majiko ya gesi ili kupunguza matumizi ya mkaa ambayo yamekuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira.
Hayo yalisemwa jana katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe wakati wa ufunguzi wa warsha ya wadau kujadili namna na njia bora ya kupunguza matumizi ya mkaa kwa usimamizi endelevu wa mazingira nchini.
Waziri Mkuu amesema nchi inakabiliwa na changamoto kubwa za uharibifu wa mazingira kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ufugaji wa kuhamahama, mifugo kuvamia misitu na kuiharibu pamoja na vyanzo vya maji na watu kukata miti katika vyanzo hivyo.
Amesema mabadiliko ya tabianchi yamesababisha mabadiliko ya vipindi vya mvua, mtawanyiko wa kiwango cha mvua na hivyo kutishia usalama wa chakula na ukosefu wa malighafi kwa viwanda ambavyo ndiyo njia ya kuivusha nchi kuingia katika uchumi wa kati.
Amesema takwimu zinaonesha asilimia 90 ya nishati ya kupikia hasa mijini ni mkaa na kwa vijijini asilimia kubwa na wananchi wanatumia kuni ambapo takwimu hizo pia zinaonesha ili kuzalisha tani moja ya mkaa sawa na magunia 30 zinahitajika tani 12 za kuni na hali hiyo imesababisha nchi kupoteza zaidi ya hekta 370,000 kila mwaka.
Amesema utafiti pia umebainisha kwamba matumizi ya mkaa yanaongezeka kutokana na ongezeko la watu na kama haitaanza kutumika nishati mbadala, mahitaji ya mkaa yatafikia takribani tani milioni tano kwa mwaka ifikapo mwaka 2030 kutoka tani milioni 2.4 zilizotumika mwaka 2015.