Waziri MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amelitaka Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), lianze kufanya tathmini ya kisayansi kuhusu manufaa ya Mifuko yote ya uwekezaji nchini ili kujiridhisha endapo inawanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.

Pia amelitaka baraza hilo lifanye tathmini kuhusu namna ya kuunganisha mifuko hiyo bila ya kuathiri majukumu ya msingi na mantiki ya kuanzishwa kwake, ili inayofanya kazi zinazofanana iunganishwe .

Ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Aprili 18, 2017) wakati akifungua maonesho ya mifuko ya uwezeshaji katika uwanja wa Mashujaa mjini Dodoma. Amesema uzinduzi wa maonesho hayo ni fursa nzuri kwa wananchi kuweza kudadisi kuhusu huduma zitolewazo na Mifuko hiyo na kutoa ushauri, ili kuboresha huduma.

Aidha, Waziri Mkuu amesema mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi yanayofanywa na Serikali yanalenga kuwawezesha Watanzania wengi wafanye shughuli za kujiongezea kipato bila kusumbuliwa na baadhi ya Watumishi wasio waadilifu.

Ameongeza kuwa “uwezeshaji wananchi kiuchumi ni jambo ambalo lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 – 2020/2021,”.

Amesema kuwawezesha wananchi kiuchumi, sio ubaguzi wala upendeleo, bali ni jitihada za makusudi za kuwashirikisha wananchi walio wengi ambao kwa sababu za kihistoria, wamejikuta wakiwa nje ya mfumo rasmi wa kiuchumi, hivyo kubaki kwenye hali duni jambo ambalo ni hatari kwa ustawi na usalama wa nchi.

Waziri Mkuu amesema jitihada za uwezeshaji wananchi kiuchumi zilizoanza tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza na kuendelezwa na awamu zote zilizofuata, ambapo kwa sasa kuna mifuko 19 ya kuwezesha wananchi kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *