Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa siku 18 kwa mkandarasi wa umeme kwenye kiwanda cha Kiluwa Steel Group awe amemaliza kazi ya kuweka umeme mkubwa ili kiwanda hicho kianze kazi.

Ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Pwani waliofika kiwandani hapo eneo la Mlandizi wakati akikagua utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Julai 12, mwaka huu alipozuru kiwanda kwa mara ya kwanza.

Waziri Mkuu pia amesema amefarijika kusikia kuwa orodha ya watu wanaodai fidia sababu ya kupisha njia ya reli ijengwe, imeshawasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa na mwenye kiwanda yuko tayari kuwalipa mara taratibu zitakapokamilika.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema haelewi ni kwa nini mkandarasi huyo anazidi kuomba siku 14 ili kukamilisha wakati aliahidi kuwa siku 14 za awali zingetosha kukamilisha kazi hiyo.

Kuhusu fidia kwa wananchi na halmashauri ya wilaya hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa alisema wananchi waliopisha njia wanadai fidia ya Sh milioni 95.76 na halmashauri inadai Sh milioni 307.26 na kwamba jumla yote ni Sh milioni 403.

Alipotakiwa ajieleze mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Dekan Group Ltd, Desderius Luhaga ambaye amepewa kazi ya kuweka umeme na transfoma Mlandizi alisema anahitaji siku 14 ili aweze kukamilisha kazi hiyo.

Hata hivyo, Kiluwa alitumia fursa hiyo kumweleza Waziri Mkuu kwamba wanapata tabu ya makaa ya mawe kwa sababu wanaletewa makaa yenye ukubwa wa milimita 10 hadi 15 badala ya milimita 35 – 40 ambazo wanahitaji kwa ajili ya kiwanda chao.

Waziri Mkuu alimwagiza Naibu Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara, John Malongo awasiliane na Wizara ya Nishati na Madini ili afuatilie ni kwa nini watengenezaji wa makaa ya mawe hawafuati vipimo halisi vinavyotolewa na wawekezaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *