Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Kassim Majaliwa ametoa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Bakari Mohammed kuhakikisha hospitali ya wilaya hiyo inakusanya mapato kwa kutumia mfumo wa kielektroniki.

Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa vyombo vya habari jana, inaonesha kwamba Waziri Mkuu amesema serikali ilishaagiza taasisi zote za umma kutumia mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato kwa lengo la kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma.

Amesema taasisi ambazo tayari zimeanza kutumia mfumo huo katika ukusanyaji wa mapato zimeongeza kiwango cha makusanyo kutoka Sh 300,000 hadi Sh milioni nne kwa siku.

Pia aliwaagiza viongozi wa wilaya hiyo kuendelea kuwahamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao utawawezesha kupata huduma ya matibabu bure katika kipindi cha mwaka mzima.

Akizungumzia kuhusu matibabu kwa wazee, Waziri Mkuu amemuagiza mkurugenzi huyo kuhakikisha anafungua dirisha la kuwahudumia wazee ili kuwarahisishia upatikanaji wa huduma wanapofika hospitalini hapo.

Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Samwel Laizer alisema mwamko mdogo wa jamii kujiunga na CHF ni moja kati ya changamoto zinazowakabili katika utoaji wa huduma za afya. Dk Laizer alisema kati ya kaya 30,000 zilizoko wilayani Nachingwea ni kaya 7,133 tu ndizo zilizojiunga na mfuko wa CHF.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *