Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe alichunguze Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na iwapo hatoridhika na utendaji wake alivunje.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Julai 5, 2017) katika hotuba yake ya kuahirisha Mkutano wa Saba wa Bunge mjini Dodoma.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano haitafumbia macho usimamizi mbovu na utawala wa michezo usiojali maslahi ya Taifa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameipongeza timu ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys iliyoshiriki na kutoa upinzani mkubwa kwenye mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika.
Amesema licha ya timu hiyo kumaliza ikiwa na jumla ya pointi 4 sawa na timu iliyoshika nafasi ya pili, ila Vijana hao wameonesha vipaji na uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yao.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua umuhimu wa michezo kwa afya, umoja wa kitaifa na kama fursa ya ajira kwa vijana nchini.
Amesema Serikali itaendelea kuratibu michezo shuleni, ikiwa ni pamoja na kusimamia ufundishaji wa michezo kama somo.