Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali itachukua hatua kuhakikisha kuwa waliohusika na mauaji ya watafiti wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian Arusha (SARI) wanakamatwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria.

Amebainisha kwamba watafiti hao waliouawa jioni ya Jumamosi iliyopita katika Kijiji cha Iringa Mvumi wilayani Chamwino katika Mkoa wa Dodoma, walifika Dodoma kutokana na agizo la serikali la kufanya uchunguzi wa matetemeko ya ardhi kama yatakuwa endelevu nchini. Mbali ya hayo, amewatoa hofu wale wanaokuja Dodoma kwa ajili ya kikazi au kuwekeza kwani Dodoma ni shwari.

Waliouawa kwa kucharangwa kwa silaha kama mapanga na shoka na kisha kuchomwa moto ni Nicas Magazine aliyekuwa de reva, mtafiti Theresia Nguma (43) na kijana aliyekuwa akianza kazi ya utafiti, Jaffari Mafuru, wote kutoka SARI jijini Arusha.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali imesikitishwa sana na tukio hilo la watumishi wa serikali kuuawa wakati wakiendelea na majukumu yao ya kazi.

 “Ni jambo la kusikitisha sana tunawaombea roho zao zipumzike kwa amani, kama serikali tutachukua hatua kwa kuhakikisha waliohusika wanakamatwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria,” alisema na kuongeza kuwa watafiti hao walitumwa na serikali kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera.

“Walikuja Dodoma kutoka Arusha kufuatia agizo la serikali la kufanya uchunguzi wa matetemeko ili ijulikane kama tetemeko ni endelevu,” alibainisha na kuongeza kuwa kufanyika kwa utafiti huo, serikali iliomba Wizara ya Nishati na Madini kupitia Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kufanyika utafiti huo, hivyo serikali kupita kwa taasisi zake iliamua kufanya uchunguzi kuhusu matetemeko hayo kama yataendelea ama la.

“Waliweka mpango kazi wapite mkoa wa kati kwenye Bonde la Ufa, walifanya kazi zao kwa siku tano siku ya sita ndipo wakakumbana na umauti. Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi,” alieleza Waziri Mkuu na kufafanua kuwa jukumu la serikali ni kuhakikisha wanaokuja Dodoma wajue Dodoma ni salama, historia ya Dodoma haioneshi kama ina matukio ya ajabu kama haya.

“Jukumu la Serikali ni kuhakikisha Dodoma ni salama, wanaokuja wataikuta Dodoma ni salama,” amesema Majaliwa ambaye alihamia mjini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita kuanza utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Tano kuhamia Dodoma kuanza sasa hadi ifikapo mwaka 2020.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *