Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali haizuii fursa ya wakulima kuuza mazao nje bali Serikali inataka mazao yatosheleze nchini kwanza kabla ya kuuzwa nje ya nchi.

Majaliwa alitoa kauli hiyo wakati akijibu hoja ya wapinzani, walioitisha mkutano wa waandishi wa habari juzi na kuilaumu serikali.

Alhamisi wiki iliyopita, wakati Waziri Mkuu akijibu swali la papo kwa hapo la Mbunge wa Viti Maalumu, Ritha Kabati aliyetaka kuruhusiwa kuuzwa mahindi nje ya nchi, alikataza kuuza mahindi nje ya nchi.

Amesema ni marufuku kuuza mahindi nje ya nchi; na kama ni muhimu lazima kibali kitoke kwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya kuuza nje ya nchi; na uuzwe unga uliosagwa na kamwe yasiuzwe mahindi.

Waziri Mkuu alitetea kauli hiyo ya serikali jana wakati akikagua banda la Ushirika wa Wakulima Wadogo wa Kilimo cha Umwagijiaji Dakawa (UWAWAKUDA) kabla ya kufunga Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD), yaliyofanyika katika Ukumbi wa CCM wa Jakaya Kikwete mjini hapa.

Alimpongeza na kumsifu mkulima Nassib Katoto kwa niaba ya wakulima wenzake wa Mpunga Dakawa mkoani Morogoro, kutokana na kulima kilimo cha umwagiliaji, lakini hasa kuvuna mpunga, kuukoboa na kuusindika ili kupata mchele na kuuweka katika mifuko na kuuza baada ya kuongeza thamani, badala ya mpunga.

Majaliwa alisema nia ya serikali si kuzuia fursa ya wakulima kuuza mahindi nje ya nchi, bali inataka kuhakikisha kila eneo nchini linakuwa na chakula, kwani baadhi ya maeneo nchini hayana chakula kutokana na kukosa mvua na hivyo kukumbwa na ukame.

Lakini, kama ni lazima kuuza chakula nje ya nchi, basi ni vema kibali kikatolewa na Waziri mwenye dhamana kwa kuuza unga badala ya mahindi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *