Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka maofisa wa Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania (TRA) wakusanye kodi za majengo kwa kuzingatia sheria na wasitoze kodi ya majengo wazee wenye umri zaidi ya miaka 60.
Waziri mkuu ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wananchi na viongozi wa Wilaya ya Chato waliohudhuria uzinduzi wa jengo la TRA wilayani humo mkoani Geita. Waziri Mkuu amewataka moafisa hao wakusanye kodi ya majengo kwenye maeneo ya mjini na siyo vijijini kwani kodi hiyo haiwahusu.
Pia aliwataka wananchi wanaonunua bidhaa wadai risiti lakini wahakikishe wanapewa risiti yenye kiwango halisi walicholipia.
Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo la ghorofa moja, Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kicheere alisema ujenzi huo ulianza Julai 12, mwaka jana na ulikamilika Juni 12, mwaka huu.
Pia alisema wamejenga ofisi hizo ili kuwapunguzia umbali wafanyabiashara wa wilaya hiyo ambao walilazimika kwenda Geita mjini kupata huduma za TRA ambako ni umbali wa zaidi kilometa 120.
Alizitaja wilaya ambazo ziko mbioni kupatiwa ofisi zake kuwa ni Kondoa, Longido, Bunda na Arumeru.
Amesema katika mwaka ujao wa fedha, TRA imelenga kukusanya Sh trilioni 17.106 na watahakikisha wanafikia lengo hilo.