Viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha imeagizwa kukaa meza moja na wawekezaji na wananchi wote wa wilaya hiyo, lengo ni kutatua kero zote zinazogombanisha pande hizo ili shughuli zifanyike kwa amani.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema hayo katika Kata ya za Ololosokwan, Piyaya na Samunge wakati alipotembelea kata hizo katika ziara yake ya siku tano wilayani Ngorongoro iliyomalizika mwishoni mwa wiki.

Gambo alisema katika maeneo yote ya wilaya hiyo kuna migogoro na malalamiko kati ya wananchi na wawekezaji na tatizo kubwa ni ushirikishwaji mdogo hivyo ni lazima jitihada za ziada zinahitaji kutatua changamoto zilizopo.

Amesema na hiyo yote imechangiwa na viongozi wa wilaya na kata na hata vijiji kukaa mbali na wananchi na kunafanya wawekezaji kushindwa kufanya kazi zao kutokana na mgogoro na wananchi, hivyo ni bora kutatua kero na kuziacha pande hizo zikilumbana na kukwaruzana bila ya sababu za msingi sio sahihi.

Amesema wawekezaji katika Wilaya ya Ngorongoro wamefanya mambo mengi makubwa kwa maendeleo ya wilaya hususan miradi ya elimu, afya na barabara na kutumia mamilioni ya fedha kusaidia wilaya, lakini kuna baadhi ya watu wanachochea wananchi na kubeza wawekezaji.

Amesema kinachotakiwa ni viongozi wa serikali ngazi ya wilaya kukaa chini na wadau wa pande zote na kuangalia matatizo yaliyopo na kutatua ili kila upande uweze kufanya shughuli zake bila ya kuingiliana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *