Serikali imesema uhakiki wa watumishi wa umma, utakamilika ndani ya mwezi huu, hivyo nafasi zilizoachwa wazi baada ya kuondolewa kwa watumishi hewa, zitaanza kujazwa.

Aidha, imesema kwamba baada ya uhakiki huo ambao utasaidia kuwa na orodha sahihi ya watumishi waliopo katika taasisi za umma kwa lengo la kuboresha hali ya utumishi nchini, itaanza mfumo wa kuhakiki majina mapya.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro alisema uhakiki wa watumishi hewa, umesaidia kuongeza ufanisi katika taasisi zake.

Dk Ndumbaro amesema baada ya kukamilika kwa uhakiki huo, pia wataanza mfumo mwingine wa kuhakiki majina mapya ambayo yatajitokeza mara mbili na kuyatoa ili kubaki na majina sahihi.

Pia amesema mfumo wa usajili kupitia Vitambulisho vya Taifa (NIDA), utasaidia kwa kiasi kikubwa, kwani utatoa taarifa sahihi za watumishi halali wa serikali.

Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imetia mkazo katika uadilifu na kwamba kauli ya Rais John Magufuli inatekelezwa ipasavyo na watumishi wa umma.

Amesisitiza kuwa kwa ujumla hali ya utumishi wa umma imeimarika tofauti na ilivyokuwa zamani na kwamba wataendelea kuwachukulia hatua watumishi watakaokiuka maadili.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *