Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amewataka baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), walioshirikiana na wenzao wa Mamlaka ya Mapato (TRA), kupitisha makontena zaidi ya 100 bila kukaguliwa na shirika hilo katika Bandari ya Dar es Salaama kujisalimisha haraka.

 

Amewataka wote wanaojijua kuhusika, kujisalimisha mapema na kutubu ili wasamehewe.

Makontena hayo yalipitishwa katika Bandari ya Dar es Salaam hivi karibuni bila ya kuthibitishwa na shirika hilo.

Waziri huyo pia aliitaka TRA kuacha kutoa makontena, bila ya shirika hilo kuthibitisha au kukagua ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini, kwa sababu mwenye mamlaka hiyo ni TBS.

Amesema watakaotubu kuwa walishiriki, waseme walishiriki vipi na lini, walishirikiana na nani na wataje sehemu yalikopelekwa makontena hayo ili serikali isaidie kukomesha hali hiyo.

Amesema anaamini kuwa waliofanya hivyo katika TRA, walifanya kwa utashi wao, bila ya ushiriki wa viongozi wao, na sasa wakati umefika wa kukomesha tabia hiyo.

Mwijage alitoa siku nne kwa wafanyabiashara waliopitisha makontena bandarini 100 bila kukaguliwa na TBS, wakatoe taarifa katika shirika. Alisema hayo baada ya kupata taarifa kuwepo kwa makontena 100, yaliyotolewa bandarini kwa siku zilizopita bila kukaguliwa na TBS.

Amesema wafanyabiashara ambao hawatajisalimisha baada ya kumalizika kwa siku hizo hatua stahiki zitachukuliwa ikiwemo kulipa faini ya asilimia 15. TBS ni miongoni mwa wadau wa bandari.

Kutokana na huduma za shehena, bandari ina wadau wakuu ambao ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Forodha, Taasisi za kudhibiti ubora wa bidhaa, TBS, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Kudhibiti Mionzi na nyinginezo.

Makontena hayo 100 yalipangwa kukaguliwa na TBS yakiwa katika Bandari Kavu (ICD), ambazo kwa mujibu wa taratibu, huhusika na kutunza mizigo inayoshushwa nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *