Watu wawili wamepoteza maisha na wengine watano kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi wakati wakiwa wamejikinga mvua chini ya mti katika kijiji cha Ntundu, Kata ya Busangi katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Muliro Jumanne amesema ajali hiyo ilitokea juzi katika kijiji hicho wakati mvua ilipokuwa ikinyesha, ndipo watu hao waliamua kujikinga kwenye mti na radi ikapiga na kusababisha vifo hivyo.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Fikiri Paschal (35) na Maneno Luzalia (16), wakati waliojeruhiwa na kupata mshituko baada ya radi kupiga ni watano ambao ni Mhoja Pasian (32), Abeli Feleshi (12), Nhungwa Jeremiah (22), Juma Mussa (16) na Paschal Mabula (11) ambaye ni mwanafunzi wa Ntundu.

Pia Kamanda huyo aliwataka wananchi kutokaa karibu na miti, hasa kipindi hiki mvua za masika zinapokaribia kuanza kunyesha kwa wingi ili kuepuka tukio kama hilo, ambalo limepoteza maisha ya watu wawili, huku akifafanua kuwa katika mfumo wa umeme ni rahisi kupata madhara, hivyo ni vema wakachukuwa tahadhari.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *