Watu wanne wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kukutwa na meno ya tembo na pembe za swala vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 197.

Washtakiwa hao ni Salum Kamota (74), Rajab Mwinyimkuu (42), Jumanne Juma (30) na Said Gunda (36). Walifikishwa mahakamani hapo juzi na kusomewa mashitaka sita.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage, Wakili wa Serikali, Elia Athanas, alidai kuwa, washtakiwa hao wanajihusisha na biashara ya nyara za serikali na walikutwa na silaha bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori na Msajili wa Silaha.

Wakili Elia alidai, katika tarehe tofauti kati ya Januari mosi na Septemba, mwaka huu katika mkoa wa Tanga na Dar es Salaam, Kamota alijihusisha na biashara ya nyara za serikali kwa kupokea na kusafirisha vipande vinane vya meno ya tembo vyenye thamani ya dola za Marekani 75,000 sawa Sh milioni 162.7 bila kibali.

Alidai katika kipindi hicho, kijiji cha Ntambabukang’ondo wilaya ya Kisarawe, Pwani, Kamota, Mwinyimkuu na Gunda, walijihusisha na biashara hiyo kwa kupokea na kusafirisha vipande vinne vya meno ya tembo vyenye thamani ya dola za Marekani 15,000 sawa na Sh milioni 32.5.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *