Watu sita wamekufa na wengine wanane wakijeruhiwa baada ya gari dogo walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka mara nne katika Kijiji cha Kipande wilayani Nkasi katika Mkoa wa Rukwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, George Kyando amesema ajali hiyo ilitokea saa 8.10 jana mchana katika Kijiji cha Kipande.

Aliwataja waliokufa kuwa ni mfungwa wa Gereza la Kitete lililopo Nkasi, Gaudensi Nyambo (27), Gasper Malimi (18) na Kenzi Mwambige (18) wote wakiwa wanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari ya Nkasi na Ofisa Mipango wa Wilaya ya Nkasi, Godfrey Mwanansao.

Amesema marehemu wawili hawajatambuliwa huku miili yote ikiwa imehifadhiwa katika chumba cha maiti katika Hospitali ya Rukwa ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga .

Amesema ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Hiace Nissan Vannette lenye namba za usajili T 966 DHP lililokuwa likiendeshwa na Lusanjo Mwaipopo aliyekimbia baada ya ajali hiyo.

Amesema gari hilo lilikuwa likitokea wilayani Nkasi kwenda mjini Sumbawanga ambapo liliacha njia na kupinduka mara nne kabla halijaanguka ndani ya gema.

Pia amesema chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika huku uchunguzi wa kipolisi ukiendelea. Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa, Dk John Lawi alisema majeruhi tisa wamepokewa hospitalini hapo ambao mmoja ambaye ni mfungwa alikufa OPD.

Aliwataja majeruhi kuwa ni pamoja na askari Magereza wa Gereza la Kitete, Fortunatus Saanane (44) aliyelazwa chumba cha uangalizi maalumu (ICU) huku hali yake ikiwa tete. Wengine ni askari Magereza, Francis Elay (30) ambaye alitibiwa na kuruhusiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *