Watu zaidi ya 21 wamekufa katika Kata ya Pinyinyi wilayani Ngorongoro mkoani Arusha kwa ugonjwa wa ajabu wa kutapika damu.

Mtendaji wa kata hiyo, James Mushi amebainisha kuwapo kwa ugonjwa huo wakati akisoma risala kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alipokwenda kutembelea kata hiyo kujionea shughuli za maendeleo, ikiwa ni ziara ya siku tano katika wilaya hiyo.

Baada ya Mushi kueleza katika risala yake juu ya kuwepo kwa ugonjwa huo kwa zaidi ya miaka minne na watu 21 kupoteza maisha, ndipo mkuu wa mkoa alipomsimamisha Mganga Mkuu wa Mkoa huo Frida Mtiki ili kupata maelezo ya kwanini mkoa haujachukuwa hatua.

Mganga huyo amesimama na kuueleza umma wa wananchi waliohudhuria mkutano huo wa hadhara kuwa hana taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa huo na wala mkoa hauna taarifa juu ya kuwepo kwa ugonjwa huo.

Majibu hayo yalimchanganya na kumkasirisha mkuu wa mkoa na kuamua kumsimamisha Mganga wa Wilaya ya Ngorongoro (DMO), Omari Sukari kutoa majibu kama na yeye hana taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa huo.

Sukari alikiri kuwepo kwa ugonjwa huo na kweli umeua watu 21 na amefanya jitihada na ziada kwa kupeleka sampuli Wizara ya Afya kwa wataalamu, kwani hata yeye ameshindwa kujua nini chanzo cha ugonjwa huo na kinasababishwa na kitu gani.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *