Jeshi la Polisi mkoani Tanga linawashikilia watu kumi (10)  kwa tuhuma za kukutwa na kilo zaidi ya 200 za dawa za kulevya aina ya heroin, mirungi na bangi.

Pia Jeshi hilo limekamata milipuko iliyokuwa imefichwa katika sehemu ya chini ndani ya begi moja dogo la kubeba mgongoni pamoja na nguo za watuhumiwa hao.

Inadaiwa ililengwa kutumiwa katika shughuli za uvuvi haramu katika maeneo ya wilaya za Mkinga, Tanga, Muheza na Pangani zilizopo kwenye ukanda wa Bahari ya Hindi mkoani humo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Tanga kuwa “watu hao tuliwakamata Februari 24, mwaka huu majira ya saa mbili usiku huko katika maeneo ya wilayani Mkinga baada ya kupata taarifa zao kutoka kwa raia wema.”

Kamanda Wakulyamba amebainisha kwamba ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi kwa mwananchi kumiliki au kusafirisha aina yoyote ya milipuko kinyume cha taratibu na kusisitiza kwamba watuhumiwa watafikishwa kwenye vyombo vya sheria mara baada ya uchunguzi kukamilika.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *