Watoto watatu wa Shule ya Msingi Lucky Vincent waliokuwa majeruhi wa ajali iliyotokea Karatu na kwenda kutibiwa nchini Marekani wamewasili asubuhi hii katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) mjini Arusha.
Watoto hao ambao ni Doreen, Sadia na Wilson waliokuwa wakitibiwa katika Hospitali ya Mercy, Sioux City, Marekani tayari wamewasili kwa ndege ya Samaritan’s Purse wakitokea nchini humo baada ya kupata nafuu.
Mamia ya wakazi wa Arusha, ndugu, jamaa, marafiki na viongozi mbalimbali wa serikali wamefika kwa ajili ya kuwapokea watoto hao.
Baadhi ya viongozi hao ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, Mbunge Lazaro Nyarandu makatibu tarafa wa mikoa na viongozi wa wilaya za mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.
Watoto hao ni miongoni mwa wanafunzi wa shule ya Lucky Vincent walionusurika kifo katika ajali ya gari iliyotokea mkoani Arusha mwezi Mei mwaka huu, ambapo inakadiriwa idadi ya waliopoteza maisha ni 33 ikijumuisha wanafunzi na walimu waliokuwa katika gari hilo.