Watanzania 18 wanaofanya kazi kwenye kampuni ya malori ya mizigo ya Alistair wametekwa na waasi nchini Congo.
Meneja usimamizi wa Tanzania na DRC wa kampuni ya Alistair , Anna Joyce Mbise madereva hao walitekwa asubuhi ya Juni 29, baada ya mapambano kati ya askari wa Serikali ya Congo na waasi hao.
Pia amesema kampuni hiyo imewasiliana na viongozi husika wa Serikali kwa kuandika barua Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ili wasaidie madereva hao kuachiwa huru wakiwa salama.
Kwa upande wake Mratibu wa Shirikisho la Wasafirishaji Afrika Mashariki (FEARTA), Emmanuel Kakuyu alisema taarifa walizonazo ni kwamba madereva hao wamekumbwa na mkasa huo katika eneo la kijiji cha Lulimba kilichopo kati ya Ziwa Tanganyika na Kindu Manyema.
Amesema waasi hawa hawajawadhuru madereva hao, lakini alifafanua kuwa madereva watatu kati ya 21 wanatoka Uganda.
Umbali kati ya Lulimba na Kigoma ni kilomita 448, lakini ili ufike Lulimba ni lazima ulizunguke Ziwa Tanganyika upande wa mashariki mwa DRC.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa dawati la Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Suleiman Saleh alijibu kwa kifupi kwamba wamepokea taarifa za utekaji huo na tayari wameanza kushughulikia.