Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili ameliagiza jeshi la polisi kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wazazi na walezi ambao watoto wao wanajihusisha na ajira za migodini.

Bupilipili amesema agizo hilo linahusisha wamiliki wa migodi ambao wamekuwa na tabia ya kuwaajiri watoto na kuwatumikisha biashara au kufanya kazi mbalimbali za ndani badala ya kuwapeleka shule.

Amesema mtoto anapaswa kusoma shule na siyo ajira, hivyo haiwezekani wazazi kuwatumikisha watoto ili wapate riziki kwa kisingizio cha hali ngumu ya maisha.

DC huyo amesema watoto  hata wakiwa kwenye ajira hawana uwezo kujadiliana  na mwajiri kupata malipo stahiki lakini pia ni kinyume na sheria.

Bupilipili  pia alitangaza kufunguliwa  mgodi  wa Kamkenga ambao ulifungwa kwa takribani wiki moja kupisha  ukaguzi wa usalama  wa mgodi.

Amesema  shughuli  za uchimbaji ziliruhusiwa katika  maduara 22 yaliyothibitishwa  kuwa  salama na mengine 44 yakiagizwa kufanya marekebisho kadhaa  kabla ya serikali kuruhusu shughuli hizo kuendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *