Watafiti  wawili na dereva mmoja wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian (SARI) jijini Arusha wameuawa na kisha miili yao kuchomwa moto katika kijiji cha Iringa Mvumi wilayani Chamwino katika mkoa wa Dodoma wakati wakifanya utafiti wa udongo, baada ya kuhisiwa kuwa ni wanyonya damu.

Waliouawa wametajwa kuwa ni Nicas Magazine aliyekuwa dereva wa gari aina ya Toyota Hilux Double Cabin lenye namba za usajili STJ 9570 mali ya Selian pamoja na watafiti wawili ambao ni Teddy Lumanga na Jaffari Mafuru.

Polisi mkoani Dodoma inawashikilia wanakijiji 30 wa kijiji cha Iringa Mvumi kuhusu mauaji hayo, huku Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana akitoa amri ya kuwasimamisha kazi Ofisa Utumishi wa Wilaya hiyo na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji ili kupisha uchunguzi wa tukio hilo.

Mauaji hayo yalitokea juzi katika kijiji cha Iringa Mvumi, tarafa ya Makang’wa wilayani Chamwino baada ya watu hao waliokuwamo katika gari hilo kuvamiwa na wanakijiji wa Iringa Mvumi na kuwakatakata kwa mapanga pamoja na silaha za jadi kisha kuwachoma moto hadi kufa. Inadaiwa chanzo cha tukio hilo ni Cecilia Chimanga (34) kupiga yowe kijijini kuwafahamisha kwamba ameona watu anaohisi ni wanyonya damu (mumiani).

Baada ya taarifa hizo kufika kijijini ndipo Mchungaji wa madhehebu ya Kanisa la Christian Family, Patrick Mgonela (46) alikitangazia kijiji kupitia kipaza sauti cha kanisani kuwa wamevamiwa na wanyonya damu ndipo wanakijiji wakaenda kuchoma gari, kuwaua na kuwachoma moto.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *