Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Jaji Joseph Warioba amewataka watanzania wote kuungana na kujiaandaa kukabiliana na baa la njaa ambalo huenda likatokea hapa nchini.
Warioba amekiri kuwa tatizo la upungufu wa chakula kwa mwaka huu ni kubwa kuliko kama ilivyozoeleka.
Ameyasema hayo leo wakati akizindua kongamano la ‘Wanawake na Uongozi’ katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam.
Jaji Warioba amesema hakuna haja ya watanzania kubishana na kulumbana kama kuna njaa au upungufu wa chakula, bali kujiandaa ikiwa ni pamoja na kujifunza kujifunza katika nchi ambazo tatizo hilo limetokea ikiwemo Kenya na Somalia.
Kuhusu vita dhidi ya dawa za kulevya, Warioba ametaka elimu itolewe kwa watu wanaojishughulisha na dawa za kulevya hususani wanaolima bangi lakini pia wasaidiwe wapate njia mbadala za kuweza kujikimu ili kuachana na shughuli hizo ambazo zinaathiri asilimia kubwa ya vijana.
Ameongeza kuwa tatizo la dawa za kulevya linaripotiwa kawaida kama siyo tatizo kwa sababu limefanywa kama jambo la siasa.
Kongamano hilo lililoandaliwa na Mtandao wa Wanawake na Katiba, ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, na limetumika pia kuzindua kitabu chenye jina ‘Nguvu zetu, Sauti zetu, Ajenda katika mchakato wa katiba mpya’ kilichoandaliwa na mtandao huo jijini Dar es salaam.