Wanajeshi wa Kenya wanatarajia kujiunga tena na Ujumbe wa kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini baada ya kujiondoa mwaka jana kutokana na utata.

Taarifa kutoka Ikulu ya Rais wa Kenya imesema kuwa Umoja wa mataifa pia umekubali kuikabidhi tena Kenya uongozi wa majeshi hao.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guteress walikutana mjini Addis Ababa, Ethiopia ambapo kongamano la Umoja wa Muungano wa Afrika AU linaendelea.

Kulingana na taarifa yake Msemaji wa rais Manoah Esipisu, wawili hao walikubaliana kurejesha uhusiano mwema ulioko kabla ya Kenya kujiondoa mwezi Novemba mwaka jana.

Umoja wa mataifa ulimtimua Kamanda wa Ujumbe, Luteni Jenerali Johnson Mogoa Ondieki aliye Mkenya, kufuatia ripoti kwamba wanajeshi wa umoja wa mataifa walichelea kuingilia kati huku raia na wafanyikazi wa misaada wakishambuliwa mjini Juba, Sudan Kusini.

Kenya ilisema uamuzi huo haukuwa wa haki na ikaamua kuondoa wanajeshi wake 1500 pamoja na kujiondoa kabisa kwenye shughuli za kutafuta amani nchini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *