Wanafunzi 35 wa shule za sekondari na wawili wa shule za msingi katika Halmashauri ya Mji wa Bunda, Mara wamekatisha masomo yao kwa sababu ya kupewa mimba.

Hayo yamebainishwa jana kwenye kikao cha wadau wa elimu kwa jili ya kuzungumzia masuala mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Mji wa Bunda.

Katika kikao hicho, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, Masalu Kisasila aliwasimamisha walimu wa shule mbalimbali na kuwataka kila mmoja ataje hali ya mimba kwenye shule yake, ambako kila mwalimu alitaja idadi ya wanafunzi ambao tayari wamepatiwa ujauzito huo.

Baada ya kazi hiyo, baadhi ya walimu hao, maofisa watendaji, pamoja na wenyeviti wa bodi na kamati za shule walithibitisha kuwepo kwa hali hiyo na kwamba wameshachukuwa hatua ikiwa ni pamoja na kufungua kesi polisi na kuwafukuza shule wanafunzi hao.

Kisasila alifafanua kuwa shule hizo ni pamoja na Sekondari ya Bunda, Nyiendo, Rubana, Sazira, Wariku, Guta, Sizaki, Kabasa, Kunzugu, Dk Nchimbi na Shule ya Wasichana ya ACT, na kwamba shule za msingi ni Mugaja na Majengo ambako kila moja ina mwanafunzi mmoja.

Alisema shule ya sekondari inayoongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi waliopatiwa mimba ni ya Sekondari ya Bunda ambayo kuna wanafunzi wanane, ikifuatiwa na Sazira yenye wanafunzi watano, huku Kabasa na Wariku kila moja ikiwa na wanafunzi wanne.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili alitaka hatua madhubuti zichukuliwe na kila mdau wa elimu wilayani hapa ili kukomesha vitendo hivyo, akieleza kuwa baadhi ya viongozi wakiwemo watendaji na wazazi wa pande zote mbili wamekuwa wakiharibu ushahidi wa kesi hizo, ikiwa ni pamoja na kutotoa taarifa kwenye vyombo husika.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *