Mwenyekiti wa Kijiji cha Iringa Mvumi Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Albert Chimanga na watu wengine 12 wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini, wakikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya waliokuwa watafiti wa Kituo cha Utafiti wa kilimo cha Serian (SARI) jijini Arusha.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na ndugu watatu wa Chimanga ambao ni Cecilia Chimanga, Julius Chimanga na David Chimanga.

Wengine ni Dorca Mbehu, Edna Nuno, Grace Msaulwa, Juma Madehe, Sosthness Mseche, Lazaro Kwanga, Yoram Samamba, Edward Lungwa na Simon Samamba.

Washitakiwa hao walifikishwa kwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini, Joseph Fovo na kusomewa shitaka lao na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Beatrice Nsana.

Ilidaiwa kuwa Oktoba 1, mwaka huu, katika kijiji cha Iringa Mvumi wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, washitakiwa waliwaua watu watatu wakiwemo watafiti wawili wa Kituo cha Utafiti cha Kilimo (SARI) jijini Arusha.

Waliouawa walitajwa kuwa ni Nicas Magazine aliyekuwa dereva na watafiti wawili Teddy Lumanga na Jafari Mafuru.

Washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji, hivyo walipelekwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Oktoba 31, mwaka huu.

Oktoba Mosi, mwaka huu watafiti waliuawa kisha miili yao kuchomwa moto baada ya kuhisiwa kuwa ni wanyonya damu.

Watu waliouwa walikuwa kwenye gari lenye namba za usajili STJ 9570 aina ya Toyota Hilux Double Cabin mali ya SARI Arusha.

Awali, ilidaiwa wanakijiji wa Iringa Mvumi waliwakatakata watafiti hao kwa mapanga pamoja na silaha za jadi, kisha kuwachoma moto hadi kufa. Chanzo cha tukio hilo ni mwanamke mmoja, Cecilia Chimanga kupiga yowe kijijini kuwafahamisha kwamba ameona watu ambao anawahisi ni wanyonya damu (mumiani).

Baada ya taarifa hizo kufika kijijini, ndipo Mchungaji wa madhehebu ya Christian Family Church, Patrick Mgonela (46) anadaiwa kukitangazia kijiji kupitia kipaza sauti cha kanisani kuwa wamevamiwa na wanyonya damu, ndipo wanakijiji wakaenda kuchoma gari na kuwaua na kuwachoma moto

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *