Watu saba kati ya 12 wamefikishwa mahakamani mkoani Morogoro kwa kosa la kumjeruhi kwa kumchoma mkuki mdomoni na kutokea shingoni mkulima Augustino Mtitu siku mbili zilizopita.

Watuhumiwa hao wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro wote wakazi wa kitongoji cha Upangwa wilayani Kilosa.

Kwa upande wake kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amesema kuwa msako uliofanywa na polisi na kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao baada ya kutokea kwa tukio hilo Desemba 25.

Kamanda huyo Matei amesema katika msako huo watu 12 walikamatwa na saba kati yao tayari wamefikishwa mahakamani. Wengine watano watafikisha mahakamani baada ya kukamilika kwa uchunguzi.

Mbali na Mtitu aliyejeruhiwa na bado anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro majeruhi wengine ni George Andrew (68) aliyejeruhiwa kichwani.

Wengine ni Yohana Wisa (26) aliyejeruhiwa mkono wa kulia, Mathayo Elia (34) aliyejeruhiwa kichwani na bega la kushoto, Josephat Mtitu (55) aliyejeruhiwa begani na shavuni na mwingine ni Paulo Thomas (56) aliyejeruhiwa mbavu na mkono wa kushoto.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *