Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watu 15 waliokaidi amri ya kuhama katika maeneo ya mabondeni.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Simon Sirro alisema watu hao wamekamatwa na Jeshi hilo kwa kushirikiana na viongozi wa Manispaa ya Ilala.

Amesema hatua hiyo ilitokana na kuendeshwa kwa operesheni ya kuwakamata watu wote wanaoendelea kuishi katika maeneo hatarishi ya mabondeni Buguruni, Kata Vingunguti.

Sirro amesema katika operesheni hiyo inayoendelea kufuatia kukiukwa kwa amri ya Mahakama ya kuwataka watu hao kuhama maeneo hayo hatarishi kufuatia kuwepo kwa mvua zinazoendelea na kusababisha mafuriko, watu hao walikamatwa huku wengine wakiendelea kutafutwa baada ya kukimbia.

Pia amewataja watu waliokamatwa kuwa ni Mohamed Hatibu, Mwanaidi Mwinyimvua, Kurwa Anthony, Mwanahamis Ally, Sophia Mwinjuma, Salim Juma, Mwajuma Athumani, Saada Saidi, Sabahi Abdallah, Mariam Abbasi, Ashura Petro, Fitina Mohamed, Faudhia Juma, Magreth John na Ayub Abdallah.

Ameongeza kwa kusema kuwa katika mahojiano na watu hao, wamekiri kuendelea kukaa katika maeneo hayo hatarishi ya mabondeni na kuwa, wanasubiri maelekezo kutoka serikalini. Upelelezi bado unaendelea na pindi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *