Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia walimu wawili na mwanafunzi mmoja wa Shule ya Sekonda Chang’ombe (Mazoezi) kwa tuhuma za kukutwa na mtihani wa kemia wa kidato cha Sita.

Kamishna wa kanda hiyo, Simon Sirro amesema kuwa wiki iliyopita Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kutoka kwa ofisa wa Baraza la Mitihani, Aron Mweteni kuwa aliwakuta watuhumiwa wakiwa na karatasi ya maswali ya mtihani wa kemia.

Amesema kuwa baada ya kuwatilia shaka na baadae kuwatia mbaroni walifanya ufatiliaji wa awali kwa Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) ambapo ilibainika kuwa mtihani huo ni miongoni mwa mitihani inaofanywa na kidato cha sita.

Kamanda Sirro amewataja watuhumiwa hao kuwa Musa Elius na Innocent Mrutu ambao ni walimu na Ritha Mosha ambaye ni mwanafunzi.

Pia Kamanda Sirro amesema kuwa watuhumiwa hao wanaendelea na mahojiano na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani kwa mujibu sheria.

Wanafunzi wa kidato cha sita wanaendelea na mitihani ya kuhitimu ambapo inafanyika nchi nzima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *