Sheikh mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum amesema kuwa waislamu wanatarajia kufanya maandamano ya amani ya Maulidi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhamad (S.A.W) yatakayofanyika Desemba 10.

Maandamano hayo yataanzia viwanja vya Mnazi Mmoja, kuelekea barabara ya Morogoro, Msimbazi, Uhuru na Lumumba na kurudi kwenye viwanja hivyo.

Amesema viongozi mbalimbali wa dini, vyama vya siasa na Serikali pamoja na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini  wataungana na Waislamu kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume.

Amesema mgeni rasmi katika sherehe hizo atakuwa Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.

Kutokana na hali hiyo, amewaomba Watanzania wote bila ya kujali tofauti za dini, rangi au kabila, kuungana na waislamu ili kusherehekea siku hiyo kwa kudumisha amani, upendo, mshikamano na umoja, jambo ambalo linaweza kujenga taifa imara.

Sherehe hizo kitaifa zitafanyika mkoani Singida katika Kijiji cha Sheruhi ambako Mufti Abubakar Zuberi ataungana na waislamu wengine katika mkoa huo na maeneo jirani ili kusherehekea siku hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *