Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema Tanzania  ina wagonjwa wa kisukari wapatao 822,880 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015.

Ugonjwa wa kisukari ni hali ambayo hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu.

Sukari hutumiwa na mwili ili kupata nishati lishe. Ili mwili uweze kutumia sukari inayotokana na vyakula, unahitaji kichocheo cha insulini. Insulini husaidia sukari kuingia kwenye chembechembe hai ili kutengeneza nishati lishe.

Ugonjwa wa kisukari unasababishwa na kichocheo hicho kupungua au kutofanya kazi kama inavyotakiwa, hivyo kiwango cha kisukari kinabaki kikubwa kwenye damu kwa sababu sukari haikuwezeshwa kuingia kwenye chembechembe hai za mwili.

Akitoa tamko la Siku ya Kisukari Duniani inayoadhimishwa duniani kote kila Novemba 14, Waziri Ummy alisema takwimu za watoto wenye kisukari mwaka 2015 ni kati ya asilimia 15 mpaka 20 ya wagonjwa wote wa kisukari ambao wanatibiwa kwenye kliniki nchini.

Akifafanua zaidi takwimu, Ummy alisema asilimia 80 ya wagonjwa wote wa kisukari ulimwenguni wanaishi katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani mwaka huu ni “Macho yote kwenye Kisukari” na waziri huyo amesema kaulimbiu hiyo inalenga katika kuwafumbua macho zaidi wananchi kwamba kisukari ni tatizo linalopamba moto siku hata siku, hivyo nguvu ziongezwe kuhakikisha wanajikinga na tabia zinazosababisha upatikanaji wa tatizo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *