Wagombea wanaowania wadhifa wa mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika (AU) watachuana kwenye mdahalo wa kihistoria katika makao makuu ya umoja humo mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Mdahalo huo utafanyika mwendo wa saa saba unusu jioni saa za Afrika Mashariki.

Utakuwa ndio mdahalo wa kwanza kuandaliwa na AU kwa wagombea wa wadhifa huo.

Kuna wagombea watano waliojitokeza wakitaka kumrithi raia wa Afrika Kusini, Nkosazana Dlamini-Zuma, ambaye anastaafu Januari baada ya kuhudumu kwa miaka minne.

Mdahalo huo, ambao utaoneshwa moja kwa moja katika baadhi ya runinga, pia utapeperushwa mtandaoni.

Waandalizi wamewaomba watu kutuma maswali kwa wagombea wakitumia kitambulisha mada #MjadalaAfrika.

  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Botswana Pelonomi Venson-Moitoi
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Chad Moussa Faki Mahamat
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Equatorial Guinea Agapito Mba Mokuy
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Amina Mohamed.
  • Mjumbe maalum wa UN Jamhuri ya Afrika ya Kati, raia wa Senegal Abdoulaye Bathily.

Bi Dlamini-Zuma aliongezewa kipindi cha miezi sita mwezi Julai baada ya viongozi wa AU kukosa kuafikiana kuhusu wagombea waliokuwa wamejitokeza wakati huo.

Waliokuwa wanawania wakati huo ni aliyekuwa makamu wa rais Uganda Specioza Wandira Kazibwe, aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Botswana Pelonomi Venson-Moitoi na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Equatorial Guinea Agapito Mba Mokuy.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *