Jeshi la Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia wafanyakazi wanne wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mwananyamala kwa tuhuma za kufanya upasuaji kwenye mwili wa maiti na kuchukua madawa ya kulevya kisha kuyauza.
Hayo yamebainshwa na Kamanda wa Kanda hiyo, Simon Sirro wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Kamanda Sirro amesema kuwa wafanyakazi hao walipasua mwili wa Mghana ambaye alikufa katika nyumba ya kulala wageni inayoitwa Red Carpet iliyopo Sinza jijini Dar es Salaam.
Baada ya mwili huo kupelekwa monchwari ya hospitali ya Mwananyamala wafanyakazi wa monchwari hiyo walipata taarifa kuwa Mghana huyo alikuwa ana madawa ya kulevya tumboni mwake ndiyo wakafanya upasuaji huo na kuchukua madawa hayo na kuyauza.
Sirro amesema kuwa baada ya jeshi la polisi kuwahoji watuhumiwa hao wamekiri kwamba ni kweli walihusika kuupasua mwili huo na kuchukua kete za madawa baada ya hapo waliyauza madawa na huyo waliyemuuzia amekwishakamatwa.
Kamanda Sirro amesema kuwa watuhumiwa hao wamekiri madawa hayo kuyauza kwa jamaa mmoja anayeitwa Ally Nyundo ambaye yumo kwenye orodha ya wauza madawa waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda.