Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imewaachia huru wabunge watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka ya kuomba rushwa ya Sh milioni 30.

Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage aliwaachia huru washitakiwa hao baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kuwasilisha hati ya kuwafutia mashitaka.

Wabunge hao ni Kangi Lugola wa Mwibara mkoani Mara, Suleiman Saddiq (Mvomero – Morogoro) na Victor Mwambalaswa (Lupa – Songwe).

Awali Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi akisaidiwa na Wakili Emmanuel Jacob kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), waliieleza mahakama kuwa kesi hiyo imetajwa kwa ajili ya washitakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Kishenyi alidai mbali na kutaka kuwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao, DPP anaomba kuwafutia mashitaka yao kwa kuwa hana nia ya kuendelea na mashitaka dhidi yao.

Baada ya maelezo hayo, Wakili wa Utetezi, Mpale Mpoki aliiomba mahakama itoe agizo ili apewe maelezo ya mlalamikaji.

Hakimu Mwijage alisema, mahakama imekubali ombi la DPP hivyo kuanzia sasa wabunge hao wapo huru.

Aidha, alisema wakili Mpoki anatakiwa afanye juhudi kwenda katika ofisi za DPP ili kupata taarifa hizo, kinyume cha hapo mahakama haiwezi kutoa amri kwamba apatiwe maelezo hayo.

Baada ya washitakiwa hao kuachiwa huru, ndugu na marafiki wa wabunge hao waliokuwa wamefika mahakamani, walianza kuangua kilio cha furaha.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge wenzake, Lugola alisema watakaa na wanasheria hao ili wajue nini cha kufanya kutokana na udhalilishaji waliofanyiwa na Takukuru.

Alisema walikuwa wanajua kuwa kesi hiyo ni ya kutunga na ilijaa siasa kwa kuwa awali Takukuru ilisema upelelezi umekamilika, lakini hawakuwa na ushahidi na ndio maana wameamua kuifuta.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *