Wabunge wamepitisha Azimio la kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa kazi kubwa, anayoifanya ya kulinda rasilimali za Taifa yakiwamo madini.

Aidha, wameshauri hatua kali zichukuliwe kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu kwa wote ambao kwa namna moja au nyingine, watathibitika kuwa wamehusika katika kuliingizia Taifa hasara na kuwakosesha Watanzania fursa ya kufaidika na rasilimali za madini.

Pia wabunge wametaka kupelekwa haraka kwa mikataba na sheria zote zinazohusu madini ili ziende kufanyiwa marekebisho ya kuziba mianya ya wizi wa fedha za Watanzania kupitia kodi na mapato mengine.

Azimio hilo la Bunge lilisomwa na Mbunge wa Newala Mjini, George Mkuchika (CCM), na kisha kujadiliwa na wabunge kabla ya kulipitisha kwa wengi kulikubali. Mkuchika alisema tangu Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk Magufuli ilipoingia madarakani, hatua mbalimbali zimechukuliwa kwa lengo la kuongeza mapato ya serikali na kuziba mianya ya upotevu wa mapato.

Alieleza kuwa kwa upande wa kuhakikisha Watanzania na Taifa kwa ujumla wananufaika na rasilimali za madini. Aliongeza kuwa rasilimali hizo zinaweza kutoa mchango katika uanzishaji wa viwanda, ustawi na maendeleo ya jamii, huduma za jamii, miundombinu na hali bora ya maisha kwa wananchi.

“Hivyo naomba kutumia fursa hii kuliomba Bunge hili Tukufu ambalo ni chombo cha uwakilishi wa wananchi, kuridhia Azimio la Kumpongeza Mheshimiwa Rais,” alisema Mkuchika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge.

Katika kuchangia Azimio hilo, Mbunge wa Kikwajuni, Hassan King (CCM) alisema ni lazima Taifa likubali kujisahihisha na kulinda rasilimali zake ili umma ufaidike nazo. Mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa (CCM), alisema Rais Magufuli ni mzalendo namba moja, na amegusa mioyo ya watu kabla ya kugusa mikono yao.

Kwa upande wake, Mbunge wa Temeke, Abdalla Mtolea (CUF), alitaka kuongezwa nguvu katika kulinda rasilimali za Taifa, kwani kuna uwezekano kampuni zilizotajwa kuibia nchi, zikawa zinasafirisha mapande ya dhahabu kwenda nje baada ya kuona wizi wao umegundulika.

Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM), alisema Taifa halistahili kukaa kimya kutokana na wizi huo. Kangi Lugola wa Mwibara (CCM) alisema Rais Magufuli ndiye ambaye Taifa lilikuwa likimhitaji, na kwamba kwa nini asipongezwe wakati akijitolea kufa kwa ajili ya kulinda rasilimali za nchi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *