Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo ameongoza wabunge katika kuuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA) Dkt. Elly Macha.
Akizungumza katika tukio hilo Waziri Mkuu ametoa pole kwa Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai, familia marehemu pamoja na wabunge wote.
Waziri Mkuu amesema enzi ya uhai wake marehemu Dkt. Elly alitoa mchango mkubwa na ushauri mzuri katika masuala ya elimu na uboreshaji wa maeneo ya watu wenye ulemavu.
Awali akisoma wasifu wa marehemu, Mbunge wa Iringa Mjini, Mheshimiwa Mchungaji Peter Msigwa alisema Dkt. Elly alipata ulemavu wa macho akiwa na umri wa miezi mitano baada ya kuugua ugonjwa wa surua.
Mchungaji Msigwa alisema pamoja na kuwa na ulemavu huo wa macho lakini haukuwahi kuwa kikwazo kwake kwani aliweza kufanya jambo lolote lililokuwa ndani ya uwezo wake.
Mwili wa marehemu Dkt. Elly umesafirishwa leo kwenda nyumbani kwake Usa River mkoani Arusha na anatarajiwa kuzikwa kesho nyumbani kwa wazazi wake katika kijiji cha Kirua Vunjo mkoani Kilimanjaro.
Dkt. Elly alizaliwa Juni 18, 1962 kwenye kijiji cha Kirua Vunjo mkoani Kilimanjaro, ambapo mbali na wadhifa wa ubunge pia aliwahi kuwa Mshauri Mwelekezi wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu vya Afrika Mashariki.