Wabunge wa chama cha Democratic nchini Marekani wamesema kuwa hawataudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule Donald Trump siku ya Ijumaa ijayo.
Hii ni baada ya Trump kumkosoa John Lewis, mbunge na mtetezi maarufu, mwenye sifa tele wa haki za binadamu, baada ya kuhoji uhalali wa ushindi wa Donald Trump.
Mtoa maoni mmoja wa siasa za msimamo mkali Bill Kristol, amesema kuwa Bwana Trump anampa Rais wa Urusi heshima kubwa mno.
John Lewis ni mmoja wa maspika ambaye bado angali hai kati ya waandamanaji wa kutetea haki za binadamu, waliohudhuria mkutano uliofanyika mwaka 1963 mjini Washington, na kuhutubiwa na Martin Luther King.
Amesema kuwa hatohudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Trump siku ya Ijumaa, kwa sababu hamtambui kama Rais aliyechaguliwa kwa haki kutawala Marekani.
Kumjibu, Bwana Trump alisema kuwa hayo yote anayosema Bwana Lewis, ni maneno matupu yasio na matendo, huku akimshauri kushughulikia maslahi ya watu wa Wilaya yake ya Georgia.