Wabunge wa Bunge la Uganda jana walivutana na kurushiana masumbwi katika mjadala wa muswada wa kuondoa ukomo wa umri wa urais nchini humo.

Wabunge wa kambi ya upinzani na wale wa chama tawala waliingia katika ugomvi huo uliohusisha pia kurushiana viti, baada ya mbunge mmoja wa upinzani kudai kuwa kuna mbunge wa chama tawala aliingia bungeni na bunduki.

Baada ya mgogoro huo, Spika aliagiza wabunge wote wakaguliwe. Ukaguzi huo uliondoa shaka baada ya kubaini kuwa hakukuwa na mbunge yeyote aliyekuwa na silaha.

Hata hivyo, mjadala wa kuondoa kipengele cha katiba kinachotaka mtu mwenye umri zaidi ya miaka 75 kutowania urais ulishindwa kuendelea baada ya wabunge wa upinzani kuimba wimbo wa Taifa bila kukoma, hali iliyosababisha Spika kuahirisha kikao hicho hadi leo.

Wapinzani wanaamini kuwa mjadala huo umepelekwa bungeni kwa lengo la kumpa nafasi nyingine Rais Yoweri Museveni kuendelea kutawala nchi hiyo.

Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, Museveni mwenye umri wa miaka 73 asingekuwa na sifa za kugombea urais kwenye uchaguzi ujao wa mwaka 2021.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *