Waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi nchini Kenya wamesema kuwa mchakato wa uchaguzi mchimi humo ulikuwa huru, wazi na wa haki.

Waangalizi hao wamesema kuwa uchaguzi huo ulifanywa katika mazingira ya amani na utulivu kote nchini.

Hata hivyo kauli zao zinajiri wakati ambapo matokeo ya urais wa uchaguzi huo yanaibua utata huku upande wa upinzani unaoongozwa na Raila Odinga ukidai kuwa mitambo ya tume ya kusimamia uchaguzi ilidukuliwa, madai ambayo tume ya kusimamia uchaguzi imeyakanusha.

Matamshi ya makundi ya waangalizi hawa wa uchaguzi yanatia gundi matokeo ambayo tume ya uchaguzi IEBC, imekuwa ikipeperusha kwenye mtandao wake, yakimweka mbele rais Uhuru Kenyatta wa kura milioni 8 dhidi ya kiongozi wa muungano wa NASA Raila Odinga aliye na kura milioni 6.6.

Kwenye kikao na wanahabari waangalizi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki wamesema kuwa japo kulikuwa na changamoto kadha wa kadha kama vile kuchelewa kufika kwa vifaa vya kupiga kura katika baadhi ya vituo, utaratibu wa uchaguzi ulikuwa sawa.

Pia wamesema kuwa asasi zilizohusika zilizingiatia uwazi kabla na baada ya uchaguzi mkuu, hivyo kuzingatia demokrasia.

Ujumbe huo umesema kuwa baadhi ya mawakala wao kwenye vituo vya kupigia kura waliona mchakato huo ukianza na kukamilika. Wamepongeza wadau wote na wakenya kwa kudumisha amani katika uchaguzi huu uliokamilika siku ya Jumanne.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *